Mashahidi Wawili
1Ndipo nikapewa kipimo kama fimbo, nikaambiwa, “Nenda kapime Hekalu la Mungu pamoja na madhabahu na uwahesabu watu waabuduo humo. 2Lakini usipime uwanja wa nje ya Hekalu, uache, kwa sababu uwanja huo wamepewa mataifa wasiomjua Mungu. Wao wataukanyagakanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na miwili. 3Nami nitawapa uwezo mashahidi wangu wawili watoe unabii kwa muda wa siku elfu moja mia mbili na sitini na mbili, wakiwa wamevaa magunia.”
4Manabii hao wawili ni ile mizeituni miwili na vile vinara viwili visimamavyo mbele za Bwana na mbele ya nchi yote. 5Na mtu akitaka kuwadhuru, moto hutoka vinywani mwao na kuwateketeza adui zao. Na hivyo ndivyo atakavyokufa mtu ye yote atakayetaka kuwad huru. 6Watu hawa wanayo mamlaka ya kuyafunga mawingu ili mvua isinyeshe wakati wote watakapokuwa wanatoa unabii wao. Watakuwa na mamlaka juu ya maji kuyageuza kuwa damu, na kuleta maafa ya kila aina ulimwenguni, kama wapendavyo. 7Lakini wakishamaliza kutoa unabii huo, yule mnyama atokaye katika shimo la kuzimu ata wapiga vita na kuwashinda na kuwaua. 8Maiti zao zitabaki katika barabara ya mji mkuu ambao kwa fumbo unaitwa Sodoma na Misri, ambapo Bwana wao alisulubiwa. 9Kwa muda wa siku tatu na nusu, watu wa kila kabila, lugha, taifa na rangi wataziangalia maiti zao, na hawataruhusu wazikwe. 10Watu waishio duniani watafura hia kifo cha manabii hao wawili na kushangilia kwa kupeana zawadi kwa sababu manabii hao waliwatesa watu waishio ulimwenguni.
11Lakini baada ya zile siku tatu na nusu, pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu iliwaingia, nao wakasimama; wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu. 12Kisha wale manabii wawili wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njooni huku juu!” Nao wakapaa mbinguni katika wingu, wakati maadui zao wakiwatazama. 13Wakati huo huo, kukatokea tetemeko kuu la nchi, na sehemu moja ya kumi ya mji ikaanguka. Watu elfu saba wakauawa katika tetemeko hilo na waliosalimika wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.
14Maafa ya pili yamekwisha kupita. Lakini maafa ya tatu yanakuja upesi.
Tarumbeta Ya Saba
15Kisha malaika wa saba akapiga tarumbeta yake. Na sauti kuu zikasikika mbinguni zikisema, “Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na Kristo wake, naye atatawala milele na milele.” 16Na wale wazee ishirini na wanne waketio mbele za Mungu katika viti vyao vya enzi wakaanguka kifudifudi wakamwabudu Mungu, 17wakisema, “Tunakushukuru, Bwana Mungu Mwenyezi uli yeko na uliyekuwako; kwa kuwa umeuchukua uweza wako mkuu na ukaanza kutawala. 18Watu wa mataifa walikasirika kwa kuwa wakati wa ghadhabu yako umefika. Wakati umefika wa kuwahukumu wafu na kuwapa tuzo watumishi wako manabii na watakatifu walioli tukuza jina lako, wakubwa kwa wadogo; na wakati umefika wa kuwaangamiza wale wanaoiangamiza dunia.”
19Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa na sanduku la agano lake likaonekana Hekaluni mwake. Kukatokea umeme, sauti, ngurumo na tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.