2 Yohana

1Kutoka kwa Mzee. Kwa mama mteule pamoja na watoto wake niwapendao katika kweli. Wala si mimi tu niwapendaye bali wote wanaoifahamu kweli; 2kwa sababu ya ile kweli ikaayo ndani yetu na ambayo itakuwa nasi hadi milele.

3Neema, huruma, na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo Mwana wake zitakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.

Kweli Na Upendo

4Nimefurahi sana kuona kwamba baadhi ya watoto wako wanadumu katika kweli, kama Baba alivyotuamuru. 5Na sasa, mama mpendwa, sikuandikii amri mpya, bali ile ile ambayo tumekuwa nayo kutoka mwanzo: kwamba tupendane. 6Na upendo ni huu: kwamba tuishi kwa kuzifuata amri za Mungu. Na kama mlivyosikia tangu mwanzo, amri yake ni kwamba muishi maisha ya upendo.

7Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, watu wasiokiri ya kwamba Kristo alikuja kama mwanadamu. Mtu kama huyo ni mdanganyifu na mpinga-Kristo. 8Jihadharini msije mkapoteza yale mliyoyafanyia kazi, bali mpewe thawabu kamili.

9Mtu ye yote anayevuka mpaka wa mafundisho ya Kristo, na kuyaacha, huyo hana Mungu. Na mtu anayedumu katika mafundisho ya Kristo, huyo anaye Baba na Mwana pia. 10Mtu ye yote akija kwenu bila kuwaletea mafundisho haya, msimkaribishe nyumbani kwenu, wala msimsalimu. 11Kwa maana mtu anayemsalimu anashiriki kazi zake za uovu.

12Ninayo mengi ya kuwaandikia, lakini sipendi kutumia kara tasi na wino. Badala yake ninatarajia kuwatembelea na kuongea nanyi uso kwa uso, ili furaha yetu ikamilike.