1Kutoka kwa Yakobo, mtumishi wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo. Kwa makabila kumi na mawili yaliyotawanyika ulimwenguni. Salamu:
Imani Na Hekima
2Ndugu wapendwa, mnapopatwa na majaribu mbalimbali, yahesab uni kuwa ni furaha tupu. 3Kwa maana mnafahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu hujenga ustahimilivu. 4Na ustahimilivu ukimaliza kazi yake mtakuwa wakamilifu pasipo kupungukiwa na cho chote.
5Lakini kama mtu ye yote kati yenu akipungukiwa na hekima, basi na amwombe Mungu, ambaye huwapa watu wote kwa ukarimu pasipo kulaumu, naye atapewa. 6Lakini aombe kwa imani pasipo shaka yo yote; maana mwenye mashaka ni kama wimbi la bahari ambalo husu kumwa na upepo, likitupwa huku na huku. 7Mtu kama huyo asidhani atapata kitu cho chote kutoka kwa Bwana; 8kwa maana yeye ni mtu mwenye nia mbili asiyekuwa na msimamo katika jambo lo lote.
Umaskini Na Utajiri
9Ndugu asiye na cheo afurahi kwa sababu Bwana amemtukuza; 10na tajiri afurahi anaposhushwa kwa maana atatoweka kama ua la mwituni. 11Maana jua huchomoza na kwa mionzi yake mikali hukausha mimea, na maua yake huanguka na uzuri wake hupotea. Vivyo hivyo tajiri naye atafifia akiwa katika shughuli zake.
Kujaribiwa
12Amebarikiwa mtu ambaye anavumilia majaribu, kwa sababu akisha stahimili atapewa taji ya uzima ambayo Mungu amewaahidi wale wampendao. 13Mtu akijaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu,” kwa maana Mungu hajaribiwi na uovu na yeye hamjaribu mtu ye yote. 14Lakini kila mtu hujaribiwa anapovutwa na kudanganywa na tamaa yake mwenyewe. 15Kisha tamaa hiyo ikisha chukua mimba, huzaa dhambi; na dhambi ikisha komaa, huzaa mauti.
16Ndugu zangu wapendwa, msidanganywe. 17Kila kipawa chema na kila zawadi kamilifu hutoka mbinguni, ikishuka kutoka kwa Baba wa nuru za mbinguni ambaye habadiliki kama kivuli. 18Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno la kweli, kusudi tuwe kama mavuno ya kwanza katika viumbe vyake.
Kusikia Na Kutenda
19Ndugu wapendwa, fahamuni jambo hili: kila mtu awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema wala kukasirika. 20Maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu. 21Kwa hiyo epukeni uchafu wote na uovu ambao umeenea, mkapokee kwa unyenyekevu lile neno lililopandwa mioyoni mwenu ambalo linaweza kuokoa nafsi zenu.
22Basi muwe watendaji wa neno na wala msiwe wasikilizaji tu, ambao wanajidanganya wenyewe. 23Kwa maana kama mtu ni msi kilizaji tu wa neno na wala hatekelezi alilosikia, atafanana na mtu ajitazamaye uso wake katika kioo, 24na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na mara moja husahau anavyofanana. 25Lakini mtu anayeangalia kwa makini katika sheria kamilifu, ile sheria iletayo uhuru, na akaendelea kufanya hivyo bila kusahau alichosi kia, bali akakitekeleza, atabarikiwa katika kile anachofanya.
26Mtu akidhani kuwa ana dini na huku hautawali ulimi wake, anajidanganya mwenyewe na dini yake ni bure. 27Dini iliyo safi, isiyo na uchafu mbele za Mungu Baba, ndio hii: kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao, na kujilinda mwenyewe usichafuliwe na ulimwengu.