2 Wakorintho 5

Makao Ya Mbinguni

1Kwa maana twajua kwamba kama hema hii tunamoishi tukiwa ulimwenguni itaharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba ya milele mbinguni, ambayo haikujengwa kwa mikono ya wanadamu. 2Maana sasa twaugua, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni, 3kwa kuwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tena tukiwa uchi. 4Tukiwa bado tunaishi katika hema hii tunaugua na kulemewa, kwa maana hatutaki kukaa bila nguo bali tunatamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili ile hali ya kufa imezwe na uhai. 5Mungu ndiye aliyetuandaa kwa shabaha hii, naye ametupa Roho wake kama mdha mana, kutuhakikishia mambo yajayo baadaye. 6Kwa hiyo wakati wote tuna ujasiri mkuu. Tunajua kwamba wakati tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na nyumbani kwa Bwana. 7Tunaishi kwa imani na si kwa kuona. 8Nasema tuna ujasiri na ingekuwa afadhali kuuacha mwili huu tukaishi nyumbani na Bwana. 9Kwa hiyo, kama tuko nyumbani katika mwili huu au tuko mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana. 10Kwa kuwa sisi sote inatubidi kusimama mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo. Na kila mmoja atapokea mema au mabaya, kulingana na matendo yake alipokuwa katika mwili.

Huduma Ya Upatanisho

11Kwa hiyo tukijua umuhimu wa kumcha Bwana tunajaribu kuwa vuta watu. Mungu anatufahamu fika. Tunaamini kwamba dhamiri zenu pia zinatufahamu tulivyo. 12Hatujaribu kujipendekeza kwenu tena, lakini tunataka kuwapeni nafasi mjisifu juu yetu ili muweze kuwajibu hao wanaojisifia mambo yanayoonekana badala ya mambo yaliyo moyoni. 13Kama tumeehuka, ni kwa ajili ya Mungu; lakini kama tuna akili timamu ni kwa faida yenu. 14Kwa kuwa upendo wa Kristo unatusukuma, tunaamini ya kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote kwa hiyo wote walikufa. 15Naye alikufa kwa ajili ya watu wote ili wote wanaoishi, wasiishi tena kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuka tena kwa ajili yao.

16Tangu sasa hatumtazami mtu ye yote namna ya kibinadamu, ingawaje hapo mwanzo tulimtazama Kristo kwa namna ya kibinadamu. Hatumtazami hivyo tena. 17Kwa hiyo mtu akiwa ndani ya Kristo, amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita, tazama, mapya yamekuja. 18Haya yote yanatoka kwa Mungu, ambaye kwa njia ya Yesu Kristo ametupatanisha na mwenyewe, na akatupa huduma ya upatanisho. 19Ndani ya Kristo Mungu aliupatanisha ulimwengu na yeye mwe nyewe, asiwahesabie watu dhambi zao. Naye ametukabidhi ujumbe huu wa upatanisho.

20Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Kristo, Mungu anatutumia sisi kuwasihi ninyi. Na sisi tunawasihi ninyi kwa niaba ya Kristo: mpatanishwe na Mungu. 21Mungu alimfanya yeye ambaye hakujua dhambi, awe dhambi kwa ajili yetu ili ndani yake tupate kuwa haki ya Mungu.