Maisha Yanayompendeza Mungu
1Hatimaye, ndugu wapendwa, tuliwaelekeza namna mnavyopaswa kuishi ili kumpendeza Mungu. Na kweli ndivyo mnavyoishi. Sasa tunawaombeni na kuwasihi katika jina la Bwana Yesu, mwendelee kufanya hivyo zaidi na zaidi. 2Mnafahamu maelekezo tuliyowapa kwa mamlaka ya Bwana Yesu.
3Mungu anapenda ninyi muwe watakatifu, mjiepushe na maisha ya zinaa; 4na kwamba kila mmoja wenu ajifunze kuishi na mke wake mwenyewe kwa njia ya utakatifu na heshima; 5si kwa kutawaliwa na tamaa mbaya kama watu wa mataifa wasiomjua Mungu. 6Katika jambo hili mtu asije akamkosea au kumdanganya ndugu yake. Kama tulivy okwisha kuwaambia na kuwaonya, Bwana atawaadhibu watu watendao dhambi zote za aina hii. 7Kwa maana Mungu hakutuita tutawaliwe na mawazo machafu, bali tuishi maisha ya utakatifu. 8Kwa hiyo mtu ye yote anayekataa mafundisho haya hamkatai mwanadamu bali anamkataa Mungu anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.
9Hatuna haja ya kuwaandikia kuhusu upendo kati ya ndugu, kwa maana ninyi wenyewe mmekwisha kufundishwa na Mungu mpendane ninyi kwa ninyi 10na kwa kweli mnawapenda ndugu wote wa Makedonia yote. Hata hivyo, ndugu zetu, tunawasihi mwendelee kuwapenda zaidi sana. 11Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akishughulikia mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yenu, kama tulivyowaambia. 12Kwa njia hii maisha yenu ya kila siku yatawaletea sifa kutoka kwa watu wasioamini na wala hamtahi taji kuwategemea watu wengine.
Kufufuliwa Kwa Wafu Na Kuja Kwa Bwana
13Ndugu wapendwa, hatupendi mkose kujua kuhusu wale wanaokufa, au mhuzunike kama watu wasiokuwa na tumaini. 14Tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, kwa hiyo tunaamini kwamba Mungu atawainua wale waliokufa pamoja na Kristo wakiwa ndani yake. 15Kama alivyosema Bwana mwenyewe, tunawaambieni kuwa sisi ambao tuko hai bado, tutakaokuwa hai mpaka Bwana arudi, kwa hakika hatutawatangulia wale waliokwisha kufa.
16Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka toka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu pamoja na sauti ya malaika mkuu na sauti ya tarumbeta ya Mungu; na wale waliokufa wakiwa wanamwamini Kristo watafufuka kwanza. 17Kisha sisi tulio hai bado, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu tukutane na Bwana angani. Na hivyo tutakuwa na Bwana milele. 18Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.